Uhakiki wa kazi za fasihi andishi
Riwaya: TAKADINI
Mwandishi: ben hanson
Wachapishaji: mathew bookstore and stationaries
Utangulizi
Takadini ni riwaya ambayo imelenga kuzifumbua macho jamii ambazo bado zinashikilia mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati. Riwaya hii imelenga kueleza namna ambayo mila na desturi zinavyotumika kuwakandamiza baadhi ya watu katika jamii hasa wanawake na watu wenye ulemavu mbalimbali.
Msanii amemtumia mhusika TAKADINI kuwakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi. Pia amemtumia Sekai kuwakilisha kundi kubwa la wanawake wanaonyanyaswa na kukandamizwa na mila na desturi za jamii mbalimbali.
Msanii anasisitiza kuwa kama baadhi ya watu wataelimika na kuwa na msimamo thabiti katika kukemea mila hizi kandamizi kama walivyofanya mzee Chivero, Shingai na Sekai, tatizo hili linaweza kupungua au kuisha kabisa.
Maudhui
Dhamira
Msanii amejikita katika kueleza kuhusiana na ukombozi wa kiutamaduni. Msanii anaonekana kusukumwa zaidi na suala la jamii kukumbatia mila na desturi zilizopitwa na wakati. Mila hizi zimefikia hatua ya kutishia uhai wa baadhi ya watu katika jamii. Hii inathibitika pale ambapo baada ya sekai kujifungua mtoto ambaye ni zeruzeru, mila zilieleza kuwa mtoto huyu anapaswa kuuawa lakini pia mama yake alipokataa suala la mwanae kuuliwa nae alitishiwa kuuliwa kutokana na kubishana na mila na desturi za jamii yake. Katika ukurasa wa 18 msanii anasema “......endapo wataamua mtoto auawe hata wewe utauawa kwa sababu ya kupinga sheria za kale.....”
Kauli hii inaonesha wazi namna ambavyo mila na desturi zinavyotumika vibaya. Pamoja na yote haya lakini msanii anatusisitiza kuwa kutafuta haki na usawa katika kumsaidia mtu hapana budi kutekelezwa bila kujali hatari yoyote inayoweza kutokea mbele. Hili linathibitishwa na sekai, kuwa pamoja na vitisho vya kuuawa aliamua kumsaidia mwanae asiuliwe. Msanii anaeleza “.....mtoto huyu asiye na msaada alimtegemea yeye, kama tu alitaka aishi. Katika kijiji hiki, kati ya watu wa makwati, zeruzeru hakuwa na nafasi.....” (uk. 19).
Hapa msanii anatueleza kuwa ukombozi huweza kuletwa kwa kuanzia ndani ya nafsi ya mtu kama alivyofanya sekai.
Pia katika kupambana na mila na desturi kandamizi msanii amemtumia mhusika shingai ambaye alikataa utaratibu wa kuchaguliwa mchumba na kuamua kuolewa na TAKADINI. Shingai anasema,
“....huyu ndiye mtu ninayetaka anioe. Hakuna aliyeniuliza kama nampenda Nhamo. Wewe na baba mlikuwa na hamu ya kuniozesha katika familia ya manyamombe hata matakwa yangu hayakusikilizwa..........nimechagua. Nakuomba msamaa wako mama, unaweza kuniua kama ukitaka, lakini katu kwa nhamo siendi.....”(uk.118).
Hapa msanii anatuonesha kuwa katika kuleta ukombozi lazima uwe tayari kujitoa mhanga kama walivyofanya sekai na shingai katika kuleta ukombozi wa kiutamaduni katika jamii zao. Juhudi zao zilizaa matunda kwani hata watu wengine walikiri kuwa sekai na TAKADINI wameleta mabadiliko makubwa sana katika jamii ile. Kati ya walioshudia mabadiliko yale ni Tendai ambaye anasema. “.....mmebadilisha mabo mengi kijijini hapa. Kwa sasa sifikirii kwamba kuna mtu yeyote atakayekuwa na moyo wa kuharibu watoto wachanga masope au wenye ulemavu. Ahsante nyingi kwako TAKADINI na kwa baba chivero......” (uk. ...)
Mapenzi
Msanii anazungumzia suala la mapenzi kwa undani katika riwaya hii ambapo ametuonesha kuwa kuna mapenzi ya dhati na mapenzi yasiyo ya dhati. Msanii anasisitiza kuwa mapenzi ya dhati ndiyo huweza kujenga jamii bora na iliyoshikamana katika kuheshimu haki na uhuru baina ya wanajamiikwani hujihisi kuwa wana undugu wa damu. Mapenzi ya dhati yaliyooneshwa  katika diwani hii ni baina ya sekai na TAKADINI, mzee chivero na sekai, mzee chivero na TAKADINI. Sekai kwa makwati, sekai na Pindai na shingai kwa TAKADINI.  Mfano shingai katika kusisitiza penzi lake kwa TAKADINI anasema “....huyu ndiye mtu ninayetaka anioe....unaweza kuniua kama ukitaka.....”(uk. 118). Hapa msanii anatuonesha kuwa japo TAKADINI alikuwa ni mlemavu wa ngozi pamoja na mguu bado shingai alimpenda na hata kuwa tayari kufa kuliko kutenganishwa nae.
Mapenzi ya uongo yaliyooneshwa katika riwaya hii nipamoja na yale ya makwati kwa sekai ambaye alimtuhumu sekai baada ya kujifungua mtoto ambaye ni sope.
Mila potofu
Mila potofu ni zile taratibu za jamii fulani ambazo kwa namna moja au nyingine  zinaweza kusababisha madhara kwa watu au viumbe wengine katika jamii. Katika riwaya hii msanii amelizungumzia suala hili kwa kina hasa baadhi ya jamii kuendeleza mila za kuwabagua watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino) au viungo vingine vya mawili. Katika jamii ya kina sekai hapakutakiwa kuishi mtu mwenye ulemavu wa ngozi, lakini pia baada ya sekai kuamua kutoroka kwenda katika kijiji cha Mtemi masasi bado kulikuwa watu walioamini kuwa zeruzeru nilazima wauawe. Msanii anasema “.......mtoto lazima auawe.....na mama yake pia, kama tu atakataa kutengana na mtoto wake” (uk. 35).
Mila nyingine potofu ni wazazi kawachagulia watoto wao wachumba. Hili ni suala ambalo lipo katika jamii zetu. Hali hii inathibitishwa na tendai ambaye alilazimishwa kuolewa na Mtemi masasi, katika ukurasa wa 47anasema.  “....namchukulia kama baba yangu badala ya mume wangu...” Hapa tendai anaeleza namna anavyokumbana na changamoto katika ndoa yake ambayo alilazimishwa kuwepo.
Suala la kuchagulia watoto wachumba halina budi kusitishwa kwani hutengeneza familia zisizo na furaha na maelewano.
Ujasiri
Ujasiri ni ile hali ya kujiamini katika kulikabili jambo fulani.  Msanii anasisitiza kuwa tunapaswa kuwa wajasiri ili kuweza kufanikisha jambo katika maisha. Msanii amemtumia sekai kuonesha namna ujasiri unavyoweza kufanikisha mambo kwani sekai asingekuwa jasiri angeweza kumpoteza mtoto wake wa pekee.
Pia shingai ameonesha ujasiri mkubwa katika kujikomboa katika makucha ya mila kandamizi za kulazimishwa kuolewa na mtu asiyempenda.
Ujasiri mwingine ni ule uliooneshwa na mzee chivero kuwa pamoja na kujua watu wa kijiji chake hawataki zeruzeru aishi, yeye alikubali kumpokea sekai na mwanae TAKADINI japo alikuwa sope.
Ndoa za mitara
Hizi ni ndoa zinazohusisha mke au mume zaidi ya mmoja. Katika riwaya hii msanii anaeleza kuwa ndoa hizi zimekuwa ni chanzo cha kutokuelewana na kuzua mitafaruku katika familia nyingi. Msanii amemtumia makwati ambaye alikuwa  na wake watatu ambao ni sekai, Dadirai na Rumbidzai. Ndoa hii haikuwa na maelewano mazuri kwani makwati alionekana kumpenda zaidi sekai kuliko dadirai na Rumbidzai, hali iliyoleta kutokuelewana baina yao. Msanii anasema “....baada ya kuonja vyakula hivyo, aliishia kula chakula kilicholetwa na sekai....tukio hili lilimhuzunisha sana Rumbidzai ambaye alitaka apendwe zaidi....”(uk.2).
Pia ndoa ya Mtemi Masasa ilionekana kutokuwa na maelewano kwani tendai ambaye alikuwa ni mke mdogo alionewa na kunyanyaswa na wake wakubwa ambao ni kama mama zake.
Suala la ndoa za mitara linapaswa kuangaliwa kwa undani kwani pakikosekana uadilifu huweza kuleta ugomvi utakaopelekea kuvunjika kwa ndoa hiyo au migogoro isiyo na kikomo.
Umoja na mshikamano
Umoja ni ile hali ya kuwa pamoja, mshikamano ni ile hali ya kushirikiana kinguvu na kifikra katika kutimiza azma fulani. Mwandishi anatuonesha kuwa ili kuweza kutatua matatizo makubwa yanayoikumba jamii hatuna budi kushikamana kwa umoja wetu. Katika riwaya hii mshikamano mzuri baina ya mzee chivero, sekai, Mtemi masasi, na tendai umewawezesha kuokoa maisha ya TAKADINI.
Nafasi ya mwanamke katika jamii
Katika riwaya hii msanii amemchora mwanamke katika sura tofauti tofauti. Msanii anamtazama mwanamke kama kiumbe jasiri na mwenye maamuzi magumu katika kutetea lile analolitaka. Hii inathibitika kwa  kumtazama sekai ambaye aliamua kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya kuokoa maisha ya TAKADINI. Pia msanii amemtumia shingai kuonesha ujasiri wa mwanamke katika kusimamia lile alitakalo. Shingai anasema, “huyu ndiye mtu ninayemtaka....unaweza kuniua kama ukitaka...” (uk. 116).
Mlezi wa familia, mwandishi anamchora mwanamke kama mlezi wa familia hasa watoto. Hili linathibitika kwa kumuangalia sekai ambaye alimlea TAKADINI mpaka alipokua mkubwa na kupata mke. Pia Mashingai alimzaa na kumlea shingai mpaka alipoolewa na TAKADINI. Hii inathibitisha kuwa kazi ya kulea aliachiwa mwanamke pekee. Baba shingai anasema kumwambia  mkewe, “hukumfundisha mwanao maana ya tendo hillo wewe?” (uk. 96). Kauli hii inathibitisha kuwa wanaume hawakuwa na jukumu la kulea watoto wao bali waliwaachia wanawake pekee.
Mwanamapinduzi, sekai na shingai wameonesha kuwa mwanamke ni mwanamapinduzi kwani waliweza kubadili mioyo ya watu katika mila na desturi zao. Sekai ameweza kuleta mapinduzi ya kiutamaduni tena akiwa uhamishoni. Tendai anasema, “...sasa sifikirii kwamba kuna mtu yeyote atakayekuwa na moyo wa kuharibu watoto wachanga, masope au wenye ulemavu....” (uk. )
Shingai pia alionesha mapinduzi kwa kukataa kuolewa na nhamo kama alivyochaguliwa na baba yake na kuamua kuolewa na TAKADINI ambaye ni sope.
Kwa upande wa pili msanii amemchora mwanamke kama kiumbe dhaifu asiye na maamuzi wala kuweza kuchangia mawazo yake katika jamii. Hii inaonekana katika baraza la Mtemi masasi ambapo wazee wote wa baraza walikuwa ni wanaume pekee.
Dhamira nyingine zilizojadiliwa katika riwaya hii nipamoja na..............................
Migogoro
Riwaya hii imesheheni migogoro mingi sana ikiwemo migogoro ya nafsi, migogoro ya mtu na mtu na hata migogoro ya kijamii. Baadhi ya migogoro hiyo ni pamoja na;
Mgogoro baina ya makwati na sekai, mgogoro huu ulitokea baada ya sekai kujifungua mtoto ambaye ni sope. Hali hii ilimfanya makwati kumchukia sekai hali iliyopelekea sekai kutoroka ili kunusuru maisha ya mwanae.
Mgogoro wa nafsi wa sekai mara baada ya kukaa muda mrefu bila ya kupata mtoto, mgogoro huu ulitokea hasa mara baada ya wake wenzake hasa dadirai na Rumbidzai kumsema vibaya juu ya hali hiyo ya kutopata mtoto. Mgogoro huu ulisuluhishwa mara baada ya sekai kupata ujauzito wa TAKADINI.
Mgogoro baina ya shingai na wazazi wake, mgogoro huu ulitokana na shingai kukataa kuolewa na nhamo ambaye ndiye alikuwa chaguo la wazazi wake na kuamua kuolewa na TAKADINI. Suluhisho la mgogoro huu ni baada ya shingai kutoroka na kwenda kulala na TAKADINI hatimae akapata ujauzito.
Mgogoro baina ya TAKADINI na nhamo, mgogoro huu ulitokana na hali ya nhamo kupenda kumbagua TAKADINI na hata kumpiga pasi na sababu yoyote. Migogoro huu haukupatiwa ufumbuzi hadi mwisho wa riwaya.
Mgogoro wa nafsi wa TAKADINI, mgogorohuu unaonekana katika ukurasa wa 123 na 124 ambapo TAKADINI alikuwa anaweza ni kitu gani kitatokea kama mtoto atakayezaliwa na shingai atakuwa sope kama yeye. Mgogoro huu unasuluhishwa mara baada ya shingai kujifungua mtoto asiye na ulemavu wa ngozi.
Migogoro mingine iliyojitokeza katika riwaya hii ni pamoja na,
Mgogoro wa nafsi wa tendai mara baada ya kuolewa na Mtemi masasi ambaye alikuwa na umri sawa na baba yake.
Mgogoro baina ya tendai na wake wenzake ambao walimchukulia kama mtoto.
Mgogoro baina ya chido na shingai kutokana na chido kuwa na wivu wa kimapenzi juu ya nhamo.
Mgogoro baina ya amai shingai na nhariswa baada ya shingai kutoroka na kwenda kulala kwa TAKADINI.
Ujumbe
Jamii inapaswa kuachana na mila potofu zinazopelekea unyanyasaji kwa baadhi ya makundi ya watu katika jamii kama vile walemavu nawanawake.
Suala la ndoa na kuchagua mchumba halipaswi kuingiliwa kwani ni maamuzi ya watu wawili waliopendana.
Msimamo, ujasiri, umoja na mshikamano ni mambo muhimu sana katika kutafuta ukombozi wa kiutamaduni
Walemavu wana haki ya kuishi sawa na watu wengine wasio walemavu.
Malezi ya watoto yanapaswa kusimamiwa na wazazi wote wawili na si kumuachia mama pekee.
Wanawake wanaweza kufanya mambo makubwa katika jamii hivyo wapewe nafasi ya kushiriki katika maamuzi.
Falsafa
Mwandishi anaonekana kuamini kuwa binadamu wote ni sawa hata kama wana utofauti kimaumbile. Na kila binadamu ana haki ya kuishi. Au
Mwandishi anaamini kuwa misingi ya haki na usawa haina budi kuheshimiwa kwa kila binadamu bila kujali maumbile wala jinsia yake.
Mtazamo
Mwandishi anautazama ulimwengu katika jicho la kiuyakinifu  ambapo anaona kuwa matatizo yanayoikabili jamii yanaweza kutatuliwa endapo jamii itafuata misingi ya haki na usawa kwa binadamu wote bila kubagua maumbile au jinsia.
Msimamo

Msimamo wa mwandishi ni kuwa, ili jamii iweze kuondokana na matatizo mbalimbali hasa ya kiutamaduni nilazima ifuate misingi ya haki na usawa kwa watu wote pasi na kubagua jinsia au maumbile.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FAIDA ZA JUICE YA KAROTI

FAIDA ZA JUICE YA UKWAJU